Dkt Kiiza Besigye akamatwa Uganda

Imebadilishwa: 1 Oktoba, 2012 - Saa 13:00 GMT

Kiza Besigye

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Uganda cha Forum for democratic change –FDC-kanali Kiiza Besigye, amekamatwa na polisi mjini Kampala kwa kile polisi wanasema ni kushawishi wananchi kujiunga katika maandamano haramu.

Amekamatwa katika barabara za mjini Kampala akiwa anatembea kwa miguu huku akifuatiwa na umati wa watu.

Dr Kiiza Besigye amekamatwa na askari polisi wa kuzuia fujo baada ya purukushani kati ya polisi na baadhi ya wafuasi wake.Polisi ilikuwa inamvuta kumuingiza katika karaninga ya polisi huku wafuasi wake wakimvuta kwa nje.

Hata hivyo polisi iliwazidi nguvu na kumuingiza katika gari lao na kumpeleka kituo cha polisi.

Baadaye naibu msemaji wa polisi Vicent Ssekatte aliwaambia wandishi habari kuwa Besigye amekamatwa kutokana na hatua ya kuchochea wananchi kufanya fujo.

Hatua hii imekuja baada ya Besigye na viongozi wengine wa upande wa upinzani chini ya vuguvugu la 4GC (For God and My country) kutangaza mwishoni mwa juma kuanzisha walichoita mchakato wa matembezi ya uhuru- Walk to freedom kupinga walichoita ufisadi, utawala mbaya na mengine. Ilikuwa imepangwa kuanza Jumatatu.

Lakini polisi walikuwa wamepiga marufuku maandamano na mikutano yote ya hadhara hadi Oktoba 10 baada ya sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya uhuru.

Wengine waliokamatwa ni Meya wa jiji la Kampala Elias Lukwago ambaye alizuiliwa nyumbani kwake.Lukwago ni mwanachama wa chama cha upinzani cha Democratic Party DP.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.