Wenye simu ghushi mashakani Kenya

Imebadilishwa: 1 Oktoba, 2012 - Saa 09:50 GMT

Simu ya rununu

Wateja milioni 2.5 wa Simu za rununu leo wamejipata mashakani baada ya Tume ya Mawasiliano nchini Kenya kuzima simu ghushi.

Zoezi hilo la kuzima simu lilianza kutekelezwa usiku wa manane na linalenga kukabiliana na uingizaji wa simu bandia, suala linalohujumu juhudi za kuimarisha usalama.

Hatua ya kuzima simu ghushi na ambayo imethibitishwa na kampuni nne za huduma za simu nchini humo, inafuatia agizo la tume ya wasiliano nchini humo ambayo inataka kukabiliana na biashara haramu, wizi wa haki miliki na tisho la usalama.

Afisaa mkuu mtendaji wa tume hiyo, Francis Wangusi, alielezea kuwa hatua ya kuzima simu hizo, ambayo ilikuwa imeakhirishwa mara tatu iliweza kutekelezwa usiku wa kuamkia leo.

Tume hiyo haijashirikiana na kampuni za huduma za simu kuzima simu ghushi tu bali pia simu ambazo wateja wake hawajasajiliwa.

Hatua hii imesababisha hasare kubwa kwa kampuni za simu.

Hata hivyo tume ya CCK, imetenga bajeti ya pesa itakazotumia kugharamia hasara ya kampuni za simu ingawa wateja wa simu hizo hawatapata fidia yoyote.

Kampuni ya Safaricom, ambayo ina wateja wengi zaidi ya kampuni zote za huduma za simu za rununu nchini Kenya, imezima simughushi, 670,000 katika masaa 15 pekee.

Kampuni ya Airtel Kenya nayo imezima simu 100,000 huku yuMobile ikizima takriban simu 45,000. Kampuni ya Telkom Orange imezima takriban simu 20,000.

Nani wa kulaumiwa kwa kuingiza nchini simu bandia?

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.