Uchunguzi wa mauaji ya Marikana waanza

Imebadilishwa: 1 Oktoba, 2012 - Saa 15:40 GMT

Tume iliyoteuliwa na serikali ya Afrika Kusini imeanza uchunguzi wa mauaji ya mwezi Agosti ya watu zaidi ya arobaini katika mgodi wa madini ya dhahabu nyeupe wa Marikana.

Wengi wa waliouawa walikuwa ni wachimba madini waliopigwa risasi na polisi wanaoshutumiwa kutumia nguvu kupita kiasi katika tukio la kwanza kuwahi kutokea tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo.

Tume hiyo imekataa ombi kutoka kwa familia za wachimba madini zilizotaka uchunguzi huo uakhirishwe kwa muda wa wiki mbili ikisema kuwa kazi hiyo inahitajika kufanywa haraka iwezekanavyo.

Uchunguzi huo utaangalia pande zilizohusika na mauaji hayo, ikiwemo polisi, utawala wa kampuni ya madini, vyama vya wafanyakazi na serikali.

Pia itawachunguza watu biinafsi au hata makundi ya watu ikiwa walichochea vurugu zilizosababisha mauaji hayo.

Tume hiyo yenye majaji watatu, ikiongozwa na jaji mustaafu wa mahakama ya rufaa Ian Farlam, inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake mwezi January mwaka ujao.

Ushahidi wa video

Takriban watu 46 waliuawa katika maandamano ya wachimba migodi wa Marikana yaliyokumbwa na vurugu na ambayo yalifanyika kufuatia wiki kadhaa za maandamano

Mauaji hayo yaliyofanyika tarehe 16 mwezi Agosti, yanasemekana kuwa mabaya zaidi kuwahi kufanyika tangu kumalizika kwa enzi ya ubaguzi wa rangi mwaka 1994.

Tume hiyo itaendesha vikao vyake katika ukumbi wa Rustenburg karibu na eneo walikouawa wachimba migodi hao.

Kuna mipango ya kuweka skrini kubwa sana katika eneo la Marikana, ili kuwawezesha jamaa za waliouawa kuweza kushuhudia vikao vya tume hiyo.

Mwandishi wa BBC mjini Johannesburg,Milton Nkosi, anasema kuwa kanda ya video ya kushtua inayoonyesha wachimba migodi hao wakiuawa, huenda ikatumiwa kama ushahidi dhidi ya polisi.

Wachimba migodi wa Marikana walikubali kurejea kazini baada ya kukubali nyongeza ya asilimia 22 ya mishahara yao.

Lakini maelfu ya wachimba migodi wengine wamekataa kurejea kazini katika kile kinachoonekana kama msururu wa migomo ya migodini kote nchini Afrika Kusini tangu ghasia kukumba migodi hiyo.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.