Mkutano mkuu wa usalama Kenya

Imebadilishwa: 2 Oktoba, 2012 - Saa 15:06 GMT

Harakati za usalama Somalia

Siku chache tu baada ya wapiganaji wa kundi la Al Shabab kung'olewa kutoka ngome yao kuu ya mji wa Kismayo, tayari viongozi wa serikali ya Somalia wana matumaini ya kujenga nchi hiyo upya.

Hii ilibainika kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa umoja wa mataifa wa usalama kuhusu eneo la Afrika Mashariki katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Mkutano huo wa Nairobi uliwaleta pamoja mawaziri kutoka kanda ya Afrika Mashariki na upembe mwa Afrika, wawakilishi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na maafisa wa umoja wa mataifa.

Naibu waziri mkuu wa Somalia, Hussein Arab Isse aliambia BBC kwamba nchi hiyo, ambayo imekumbwa na vita vya kiukoo kwa zaidi ya miongo miwili, imeanza kushuhudia amani baada ya wapiganaji wa kundi la kiislamu la Al Shabab kutimuliwa kutoka Kismayo.

Mkutano huo pia uliangazia ukosefu wa usalama nchini Sudan Kusini, ambayo ilijinyakulia uhuru wake mwezi julai mwaka jana kutoka kwa Sudan.

Katika siku za karibuni, mataifa jirani yamelalamikia utawala wa rais Salva Kiir kuhusu madai ya kuteswa kwa raia wa kigeni wanaohudumu katika mji mkuu wa Juba.

Hata hivyo, waziri wa ulinzi wa Sudan kusini, Generali Loyai Deng' alijitetea vikali na kusema kwamba wameanzisha mipango mahsusi ya kuwapa mafunzo askari wa nchi hiyo.

Waziri huyo wa ulinzi alisema Sudan kusini inafanya kila juhudi kuimarisha usalama wake.

Mkutano wa Nairobi kuhusu mabadiliko katika sekta ya usalama kuhusu nchi za Afrika mashariki unafanyika siku chache tu baada kikosi cha AMISON kikiongozwa na majeshi ya Kenya na Somalia, kutwa mji wa Kismayo kutoka kwa wapiganaji wa Al Shabab.

Pia unafanyika wakati nchi za Sudan Kusini na Sudan kutia saini makubaliano kuhusu ugavi wa rasilimali na kusuluhisha migogoro ya mipaka.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.