Chelsea yasalia kileleni

Imebadilishwa: 6 Oktoba, 2012 - Saa 17:44 GMT
Wachezaji wa Chelsea wakishangilia bao

Wachezaji wa Chelsea wakishangilia bao

Mabingwa wa bara Ulaya Chelsea leo imeendeleza uongozi wake wa ligi ku ya Premier ya England, baada ya kuilaza Norwich kwa mabao 4-1.

Wachezaji hao wa Chelsea walisahau matatizo yao yanayowakumba nje ya uwanja wa kuhakikisha kuwa wamezoa alama tatu muhimu katika mechi hiyo.

John Terry na Ashley Cole, walitajwa katika kikosi cha wachezaji kumi na mmoja wa kwanza wa Chelsea, lakini licha ya kuwepo kwa wachezaji hao, Norwich ndio iliyokuwa ya kwanza kuona lango la Chelsea kupitia kwa naodha wake Grant Holt.

Chelsea, hata hivyo ilizawazisha dakika tatu baadaye kupitia kwa nyota wake Fernando Torres.

Frank Lampard alivurumisha kombora kali na kuifungia Chelsea bao lake la pili.

Juan Mata kisha akamuandalia Eden Hazard pasi nzuri ambalo alilipachika wavuni na kufikisha idadi ya magoli kuwa matatu kwa moja.

Mashambulizi ya Chelsea, hayakuishia hapo na baada ya patashika katika lango la wageni wao mcheza kiungo Branislav Ivanovic akalipachika bao la nne la Chelsea.

Matatizo ya Norwich yaendelea

Kufuatia kipigo hicho, Norwich sasa imesalia kuwa miongoni mwa vilabu ambavyo havijashinda mechi yoyote msimu huu na mkufunzi wa klabu hiyo Chris Hughton, ana wasi wasi mkubwa kuhusu hatma yake ya baadaye na tayari klabu yake imefungwa magoli kumi na saba msimu huu.

Ushindi huo wa Chelsea ni afueni kwa wachezaji wake ambao wamekuwa matatani na shirikisho la mchezo wa soka nchini Uingereza FA.

Jopo lililokuwa limeteuliwa na shirikisho hilo kuchunguza madai ya ubaguzi wa rangi dhidi ya John Terry, lilisema kuwa ushahidi aliowasilisha mchezaji huyo haukuwa na uzito, ukweli au msingi wowote.

Pia hatua ya mcheza kiungo wa Chelsea, Ashley Cole ya kutuma ujumbe kwa mtandao wa Twitter kushutumu FA, kuhusiana na madai kuwa alihusika kwenye sakata hiyo pia kulimuweka matatani.

Kufikira sasa Chelsea bado inaongoza kwenye msururu wa ligi hiyo ya England na alama 19 baada ya kucheza mechi 7.

Mabingwa watetezi, Manchester City wamesalia katika nafasi ya pili na alama 15 kufuatia ushindi wao wa mabao matatu kwa bila dhidi Sunderland. Everton nayo imesalia nafasi ya tatu na alama 14.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.