Wafungwa wa kisiasa waachiliwa Misri

Imebadilishwa: 9 Oktoba, 2012 - Saa 14:43 GMT

Rais wa Misri Mohammed Morsi

Rais wa Misri Mohammed Morsi, amewaachilia wafungwa wote waliokamatwa na kuzuiliwa tangu mwanzoni mwa mwaka jana kufuatia maandamano yaliyomwondoa mamlakani aliyekuwa Rais Hosni Mubarak.

Rais Morsi alitumia mtandao wa kijamii wa Facebook kutangaza msamaha huo kwa makosa ya uhalifu pamoja na yale madogo madogo kama ishara ya kuunga mkono mapinduzi yaliyomwondoa mamlakani Hosni Mubarak

Amri ya Rais huenda ikasababisha maelfu ya wafungwa wengine wengi kuachiliwa huru

Mubarak aliondoka mamlakani mwezi Februari mwaka jana kufuatia siku kumi na nane za maandamano ambapo maelfu ya watu waliuawa.

Mubaraka anahudumia kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia mwezi Juni kwa kukosa kuzuia mauaji hayo.

Miongoni mwa waliosamehewa ni wale waliofanya makosa madogo madogo au waliopatikana na hatia ya kuwa na nia ya kuyafanya makosa hayo kwa lengo la kuunga mkono mapinduzi ya kiraia.

Wengi wa wale waliofikishwa mahakamani walizuiliwa kwa kipindi cha miezi kumi na sita ambacho Misri iliongozwa na baraza la jeshi ambalo lilichukua mamlaka ya rais punde baada ya Mubarak, kung'atuka mamlakani.

Zaidi ya watu 12,000 walifikishwa mbele ya mahakama za jeshi wakati huo. Lakini vuguvugu la kutetea haki za wafungwa lililopinga kesi za kijeshi, limesema kuwa takriban wafungwa 5,000 wa kisiasa wangali gerezani.

Mshauri wa kisheria wa rais Mursi, Mohammed Gadallah, alisema kuwa msamaha huo ni moja ya hatua kubwa za ushindi kwa wanaharakati wa mapinduzi.

Hata hivyo, mawakili wa haki za binadamu, walisema kuwa amri ya Rais Mursi haijielezi vizuri sana na kwamba hakuna watu waliachiliwa mara moja baada ya kutangazwa.

Inasema kuwa majina ya wale waliosamehewa, lazima yachapishwe na mwanasheria mkuu pamoja na kiongozi wa mashtaka wa serikali katika kipindi cha mwezi mmoja. Wale ambao majina yao hayatachapiswha , wataruhusiwa kuhoji uamuzi wa Rais.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.