Mkuu wa mashtaka Misri akaidi rais

Imebadilishwa: 13 Oktoba, 2012 - Saa 14:13 GMT

Mkuu wa mashtaka wa Misri, AbdalMajid Mahmoud, amerejea ofisini na ulinzi mkali na hivo kukaidi amri ya Rais Mohamed Morsi ya kumtoa kazini.

Mkuu wa mashtaka wa Misri

Rais Morsi alijaribu kumtoa kazini mkuu wa mashtaka siku ya Alkhamisi baada ya afisa huyo kuwafutia mashtaka maafisa zaidi ya 40 watiifu kwa rais wa zamani, Hosni Mubarak, ambao walishtakiwa kwa kuongoza mashambulio dhidi ya waandamanaji wakati wa mapinduzi ya mwaka jana.

Mkuu wa mashtaka na wafuasi wake wanasema rais hana madaraka hayo.

Kuachiliwa kwa washtakiwa hao kulizusha maandamano ya ghasia katika medani ya Tahrir mjini Cairo Ijumaa, ambapo watu zaidi ya mia moja walijeruhiwa kwenye maandamano makubwa kabisa dhidi ya rais tangu kushika madaraka mwezi wa Juni.

Mkuu wa mashtaka, Abdel Maguid Mahmoud, alirudi ofisini mwake huku amezungukwa na walinzi na mamia ya mahakimu na mawaikili.

Alitaka kuonesha uhuru wake baada ya Rais Morsi kujaribu kumtoa kazini, kwa kumteua kuwa balozi wa Misri Vatikani.

Inaarifiwa kuwa majaji kadha walitishia kujiuzulu piya.

Tena mkuu wa mashtaka alikwenda kwenye mkutano na mmoja kati ya ma-naibu wa rais kujaribu kuzimua mambo.

Wakati wa serikali ya zamani kulikuwa na malalamiko mengi kuwa mahakimu na maafisa wa mashtaka wakishawishiwa na serikali.

Sasa, chini ya serikali mpya, wanajaribu sana kuonesha uhuru wao.

Hichi kisa kimeleta aibu kwa rais - na tayari kuna ishara kuwa anajaribu kubadilisha uamuzi wake wa kumtoa kazini mkuu wa mashtaka.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.