Mauaji ya kulipiza kisasi Mombasa

Imebadilishwa: 15 Oktoba, 2012 - Saa 13:51 GMT

Wanachama wa MRC

Afisaa mmoja nchini Kenya ameuawa katika kile polisi wanashuku ni shambulizi la kulipiza kisasi kufuatia kukamatwa kwa kiongozi wa vuguvugu la MRC (Mombasa Republican Council) mjini Mombasa, Pwani mwa Kenya

Salim Changu ambaye ni naibu chifu wa eneo hilo alinyongwa nyumbani kwake katika eneo la Kwale mjini Mombasa, kwa mujibu wa duru za polisi.

Kifo chake kinajiri baada ya kukamatwa kwa kiongozi wa vuguvugu hilo linalotaka kujitenga kwa eneo la Pwani
Oscar Mwamnuadzi. Alikamatwa baada ya ufyatulianaji risasi katika makao yake mjini humo ambapo polisi waliwaua watu wawili.

Hali ya taharuki imekuwa ikitanda huku uchaguzi mkuu ukikaribia mwezi Machi mwaka ujao.

Zaidi ya watu 100 wameuawa katika ghasia za kikabila Kusini Mashariki mwa eneo la Tana River tangu mwezi Agosti. Ghasia hizo zilisemekana kuwa mbaya zaidi kushuhudiwa tangu kutokea kwa ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007.

Msemaji wa polisi, Aggrey Adoli alisema kuwa Bwana Changu, ambaye ni naibu chifu wa eneo la Kombani, huenda aliuawa na wanachama wa MRC waliomuona kama msaliti.

Mapema wiki jana polisi walianzisha msako mkali dhidi ya wanachama wa vuguvugu hilo, kufuatia madai kuwa wanapanga kutatiza mitihani ya kitaifa.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.