Shirikisho la soka lataka uwanja Somalia

Imebadilishwa: 19 Oktoba, 2012 - Saa 14:32 GMT

Uwanja wa soka wa Mogadishu unatumiwa na vikosi vya AU

Kikosi cha wanajeshi wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, kimesema kuwa kinatumai kuondoka katika kambi yake ambayo ni uwanja wa taifa wa soka mjini Mogadishu haraka watakavyoweza.

AU imesema itaondoa vikosi vyake kabla ya mwezi Disemba wakati shirikisho la soka la Somalia litaanda michuano hapo.

Mapema wiki hii shirikisho la soka nchini Somalia, liliwataka wanajeshi wa Muungano wa Afrika kuondoka kwenye uwanja huo ili uweze kutumiwa kwa shughuli za michezo.

Uwanja wa soka wa Mogadishu, ulianza kutumiwa na wanamgambo pindi tu baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanza mwaka 1991 na umekuwa ukitumiwa kama kambi ya wanamgambo tangu hapo.

Afisaa mmoja wa shirikisho hilo, aliambia BBC kuwa ombi lake lilitolewa wakati wa ziara rasmi ya maafisa wa shirikisho hilo katika uwanja huo siku ya Jumanne.

Hali ya usalama mjini Mogadishu imeimarika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Wanajeshi wa Muungano wa Afrika na wale wa serikali ya Somalia, waliwafurusha wanamgambo wa Al-Shabab kutoka katikati mwa Mogadishu mwezi Agosti mwaka 2011.

Duru zinasema kuwa licha ya kuwa bado kuna mashambulizi ya mara kwa mara tangu wanamgambo kuondoka mjini humo watu wamekuwa wakikarabati majengo kote nchini humo.

Pia hatua zimepigwa katika nyanja za kisiasa hasa baada ya Rais mpya kuchaguliwa mwezi jana katika kile kilichosemekana kuwa uchaguzi wa kwanza kuwa huru na wa haki katika miaka 42.

Katibu mkuu wa shirikisho la soka, aliambia BBC kuwa alitembelea uwanja huo na maafisa wengine wakuu kutoka wizara ya michezo.

Alidokeza kuwa walitoa ombi la kutaka uwanja huo uliojengwa na wachina mnamo miaka ya sabini kurejeshwa katika hali yake ya zamani na kwa matuimzi yaliyonuiwa.

Lakini wadadisi wanasema kuwa uwanja huo ni muhimu kwa wanajeshi wa AU kwa sababu ya kuweza kudhibiti Kaskazini mwa Mogadishu na kwamba huenda AU ikakosa kuukabidhi kwa shirikisho hilo

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.