Jeshi Nigeria linakiuka haki za binadamu

Imebadilishwa: 1 Novemba, 2012 - Saa 13:54 GMT

Wanajeshi wa Nigeria wakishika doria

Jeshi la Nigeria limetuhumiwa kufanya vitendo vya kukiuka haki za bindamu katika harakati zao dhidi ya kundi haramu la Boko Haram.

Madai haya yametolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International.

Shirika hilo limesema katika ripoti yake kuwa ukiukwaji unaofanywa na wanajeshi ni pamoja na mauaji ya kiholela, utekaji nyara na mateso.

Msemaji wa jeshi la Nigeria amekanusha madai hayo akisema kuwa wanajeshi hufanya kazi yao kwa kuzingatia sheria.

Harakati za kundi la Boko Haram, wanaopigania sheria za kiisilamu pia zimesababisha vifo vya mamia ya watu mwaka huu.

Wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara kaskazini mwa Nigeria na maeneo ya kati mwa Nigeria mwaka 2009.

Katika ripoti yake shirika la Amnesty limelaumu Boko Haram kwa visa vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu mauaji, kuteketeza makanisa na shule na mashambulizi yao dhidi ya waandishi wa habari.

Lakini ilisema kuwa hatua za jeshi dhidi ya kundi hilo zimechochea hali ya vurugu kuwa mbaya zaidi.

" Hali ya mashambulizi na mashambulizi ya kulipiza kisasi imehusisha vurugu kutoka pande zote athari zake zikiwa mbaya zaidi dhidi ya haki za watu hususan wale walionaswa katika vita hivi’’ alisema katibu mkuu wa shirika hilo Salil Shetty.

"Watu wanaishi kwa hofu ya mashambulizi kutoka kwa Boko Haram na kufanyiwa vitendo vya dhulma mikononi mwa jeshi ambalo linapaswa kuwalinda’’ aliongeza Shetty.

Kwa mujibu wa Amnesty, visa vya watu kupigwa risasi na wanajeshi au kupigwa hadi kufa wakati wakizuiliwa ni kawaida katika eneo la Kaskazini mashariki mwa nchi.

Amnesty linanukuu kile ilichosema ni watu kuendelea kuishi kwa hofu ambapo hata wanaogopa kuripoti uhalifu na waandishi nao wanapuuza kuripoti taarifa hizo.

Amnesty Inataka serikali kuelezea ukweli kuhusu matukio ambayo yamehusisha jeshi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaofanya udhalimu huo

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.