Sema Kenya ikiwa Naivasha

Imebadilishwa: 1 Novemba, 2012 - Saa 14:41 GMT

Msimulizi wa kipindi Joseph Warungu

Jumapili tarehe 4 Novemba, kipindi cha Sema Kenya kilizuru mji wa Naivasha.

Naivasha ni mji ulioko Kaunti ya Nakuru na ambao ni maarufu sana kutokana na biashara ya kukuza maua na utalii.

Mji huu pia una viwanda mbalimbali na mradi wa kuzalisha nishati kwa kutumia mvuke katika eneo la Ol-Karia, ni mojawapo ya vivutio

Kwa kuwa mji wa Naivasha una sehemu nyingi za kuvutia watalii, hasaa hoteli za kifahari, umekuwa chaguo la wengi hasaa kuandaa warsha.

Mikutano muhimu na ya kihistoria imefanyika katika mji huu. Mfano ni mazungumzo ya kutafuta amani na maridhiano kati ya Sudan na Sudan Kusini. Na hata mchakato wa kutengeneza katiba mpya ya Kenya ulikamilika Naivasha mwaka 2010.

Hata hivyo, mji huu ulishuhudia ghasia na vurugu baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 na wengi walifukuzwa au walilazimika kuhama makazi yao na kujipata wakiwa wa wakimbizi wa ndani katika kipindi hicho.

Eneo bunge la Naivasha ni moja kati ya maeneo bunge 11 yaliyoko katika kaunti ya Nakuru.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka( IEBC), eneo bunge la Naivasha lina idadi ya wapiga kura 224,000 na kata nane.

Kero kubwa za wakazi wa mji huu wa Naivasha ni pamoja na:

Malipo duni yanayotolewa kwa wafanyikazi walioajiriwa katika mashamba ya maua. Hili linaathiri uhusiano wa wafanyikazi viwandani na waajiri wao.

Suala la maji na mazingira safi ya Ziwa Naivasha ambalo linatumiwa vibaya na viwanda vilivyo karibu linawatatiza wengi. Hali kadhalika utaratibu wa kusimamia taka pia hauwaridhishi wenyeji wa mji huu.

Ingawa Ziwa Naivasha limo pembeni mwa mji huo, kuna ukosefu wa maji safi Naivasha.

Wakaazi wengine pia wanalalamika kuwa hawana hati za kumiliki ardhi.

Sawa na sehemu zingine nchini Kenya, tofauti za kikabila na ukosefu wa ajira ni baadhi ya kero za wananchi.

Mfano unaodhihirika na malalamishi ya watu kuajiriwa kwa upendeleo kwenye mradi wa kuzalisha nishati kwa kutumia mvuke ulioko Ol-Karia.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.