Ndege ya kijeshi yaanguka Afrika Kusini

Imebadilishwa: 6 Disemba, 2012 - Saa 14:16 GMT
Pretoria

Ndege ilikuwa ikielekea kutoka Pretoria hadi uwanja wa Mthatha

Ndege ya kijeshi nchini Afrika Kusini imeanguka katika eneo la milima mashariki, ikiwa na abiria 11.

Ilikuwa ikisafiri kutoka mji wa Pretoria, ikielekea Mthatha, na iliripotiwa kutoweka siku ya Jumatano, lakini juhudi za awali za kuitafuta zilikatizwa kutokana na hali mbaya ya hewa.

Mabaki ya ndege hiyo yalipatikana katika milima ya Drakensberg, karibu na mji wa Ladysmith, katika mkoa wa KwaZulu-Natal.

Maafisa wa serikali wamekanusha taarifa za awali kwamba kundi la matabibu wa Nelson Mandela walikuwa ni miongoni mwa abiria katika ndege hiyo.

Akizungumza na BBC, msemaji wa idara ya ulinzi nchini Afrika Kusini, Xolani Mabanga, alikanusha uvumi wa awali kupitia vyombo vya habari kwamba ndani ya ndege hiyo walikuwemo madaktari wa rais wa zamani.

Kulingana na shirika la habari la AP, Brigedia Generali Mabanga alisema ndege hiyo ilipaa kutoka kituo cha wanajeshi wa anga cha Waterkloof mjini Pretoria usiku wa Jumatano.

Alielezea kwamba wanajeshi walitumwa katika eneo hilo kuwatafuta abiria walionusurika.

Mabaki ya ndege hiyo yalipatikana maili 210 (kilomita 340), kusini-mashariki mwa kituo cha wanajeshi cha Waterkloof.

Mabaki hayo, ya ndege hiyo aina ya Douglas DC-3 Dakota, yalitawanyika katika eneo kubwa la mahali maarufu milimani panapojulikana kama Giant's Castle.

Uwanja mdogo wa ndege wa Mthatha umo katika mkoa wa mashariki, Eastern Cape, maili 17 (kilomita 30) kutoka nyumba ya kijijini ya Mandela, Qunu, alikoamua kuishi tangu kuachana na huduma za umma baada ya kustaafu.

Jeshi la nchi hiyo lina wajibu wa kumtunza kiafya rais huyo wa zamani, ambaye sasa ametimia umri wa miaka 94.

Kulingana na shirika la habari la AP, ndege nyingine ya kijeshi ilifanikiwa kutua, licha ya kupata ajali mwezi Novemba, na watu kadha walijeruhiwa.

Jeshi wakati huo lilitangaza kwamba waliojeruhiwa hawakuwa na uhusiano wowote na matabibu wa Bw Mandela.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.