Mkutano wa hali ya hewa wazidishiwa muda

Imebadilishwa: 8 Disemba, 2012 - Saa 15:01 GMT

Mkutano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa umeendelea ingawa ukitarajiwa kumalizika Ijumaa.

Jumba la mkutano wa hali ya hewa mjini Doha, Qatar

Kumetokea mabadiliko jana usiku na kuna uwezekano wa mataifa tajiri kutakiwa kuzilipa nchi masikini kwa hasara inazopata kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Marekani imepinga vikali hatua zilizopendekezwa - inasema gharama zake zitakuwa hazina kikomo.

Lakini baada ya mvutano katika majadiliano ya usiku kucha, swala la "Hasara na Uharibifu" sasa liko katika sehemu ya mwisho ya majadiliano.

Nchi ndogo za visiwa ambazo zinakabili hatari ya kugubikwa na maji, zinasema zitatoka kwenye mkutano huo unaofanywa Doha, Qatar, iwapo Marekani itapiga kura kukataa makubaliano yanayopendekezwa.

Kisiasa makubaliano hayo ni muhimu sana.

Msimamo wa Umoja wa Ulaya bado haujulikani wazi.

Marekani inataka iungwe mkono na mataifa mengine yanayofanya uharibifu mkubwa wa mazingira, kama Canada.

Mataifa kama hayo yanaweza kubeba mzigo mkubwa wa kulipa fidia kwa uharibifu huo.

Ikiwa Marekani itaachwa peke yake kupambana na makubaliano hayo, basi wajumbe wake watakuwa na mtihani mkubwa.

Ama wakubali kauli ya wengi na wakiri kuwa mataifa yaliyosababisha mabadiliko ya hewa yawajibike kwa nchi nyengine zinazoumia, au wakatae kutia saini.

Iwapo Marekani itapinga makubaliano basi Rais Obama ataonekana kuwa ameshindwa na hana msimamo thabiti kwa sababu wakati wa kampeni za uchaguzi aliahidi kuwa atashughulikia mabadiliko ya hali ya hewa.

Na akikubali makubaliano wapinzani wake wa chama cha Republican watamshutumu kuwa anayapa kipa umbele makubaliano yatayoumiza uchumi wa Marekani.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.