Mamaake waziri wa fedha wa Nigeria atekwa nyara

Imebadilishwa: 10 Disemba, 2012 - Saa 08:32 GMT
Waziri Ngozi Okonjo-Iweala

Waziri Ngozi Okonjo-Iweala

Duru rasmi nchini Nigeria zimesema kwamba mamaake waziri wa fedha, Ngozi Okonjo-Iweala, ametekwa nyara.

Professor Kamene Okonjo alichukuliwa kutoka nyumbani kwake jimboni Delta Jumapili.

Taarifa kutoka wizarani ilisema kwamba Bi Okonjo-Iweala alikuwa ametishiwa hapo awali, lakini hawakuwa na uhakika iwapo tishio hilo lilikuwa na uhusiano wowote na utekwaji nyara huo.

Nigeria ni mmojawapo wa nchi zenye visa vingi vya utekaji nyara, uhalifu unaoingiza mamilioni ya fedha kila mwaka.

Siasa au fedha?

Visa vingi hutokea katika Jimbo la Delta lenye utajiri mkubwa wa mafuta, ingawaje kutekwa nyara kwa watu wakubwakubwa si kawaida.

Afisa wa usalama alisema haikujulikana iwapo sababu ilikuwa ya kisiasa au ya kifedha.

Bi Okonjo-Iweala ameongoza kampeni kubwa ya kujaribu kuangamiza ufisadi nchini Nigeria, hususan katika mpango tata wa ruzuku za mafuta.

Amechelewesha malipo kwa wanaoingiza mafuta nchini, huku akisubiri kuthibitishwa kwa ruzuku hizo.

Utekaji nyara

Lakini wadadisi wanasema kwamba utekaji nyara wenye sababu za kisisasa ni nadra sana nchini Nigeria.

Bi Okonjo-Iweala alikuwa mmojawapo wa wale waliogombea kuiongoza Benki ya Dunia katikati mwaka huu, lakini akashindwa na Jim Yong Kim.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.