Rais wa Venezuela apata nafuu

Imebadilishwa: 13 Disemba, 2012 - Saa 06:19 GMT
Rais Hugo Chavez

Rais Hugo Chavez

Serikali ya Venezuela inasema hali ya rais Hugo Chavez inazidi kuimarika baada ya kufanyiwa upasuaji nchini Cuba Jumanne. Anaugua ugonjwa wa saratani.

Lakini mawaziri wamesema kwamba siku za usoni zitakuwa ngumu kwake na itachukua muda mrefu kwake kupona. Waliwaonya wananchi wa Venezuela wajitayarishe kwa siku za baadaye zenye hali ngumu.

Chavez, mwenye umri wa miaka 58, sasa amefanyiwa upasuaji mara nne tangu alipoanza kuugua mwezi Juni 2011.

Taarifa kuhusu ni saratani ipi inayomsumbua Chavez haijawahi kutangazwa hadharani.

Maombi

Rais Rafael Correa wa Ecuador, mshirika wa karibu wa Chavez, amesema ni sharti mifumo yake ya mabadiliko nchini Venezuela iendelee, hata kama hataweza kurejea mamlakani.

Televisheni ya taifa ilirusha picha zilizoonyesha wananchi wa Venezuela wakimuombea rais kanisani.

Chavez angali nchini Cuba, na haijulikani ni lini atarejea nchini. Anatarajiwa kuapishwa rasmi kwa muhula wake wa nne kama rais katika kipindi cha mwezi mmoja ujao.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.