Maandamano makubwa kupinga ubakaji India

Imebadilishwa: 29 Disemba, 2012 - Saa 17:53 GMT
Maandamano India

Raia wa India wakiandamana

Maelfu ya watu wamejiunga katika maandamano ya amani katika mji mkuu wa India, Delhi, kupinga kitendo kilichosababisha kifo cha mwanamke mmoja ambaye alibakwa na kundi la wanaume mjini humo.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 23, ambaye bado hajatambuliwa, amekufa kutokana na na majeraha Jumamosi huko Singapore alikopelekwa kupata matibabu maalum.

Wanaume sita wanaoshikiliwa kuhusiana na tukio la kumbaka mwanamke huyo, sasa wamefunguliwa mashitaka ya mauaji.

Shambulio hilo la aibu lilifanyika tarehe 16 Desemba 2012 na kusababisha maandamano kupinga unyanyasaji wanaofanyiwa wanawake nchini India.

Maafisa wawili wa polisi tayari wamesimamishwa kazi.

Mwili wa mwanamke huyo unarejeshwa India katika mazishi yatakayofanyika kwa siri kuepusha ghasia zaidi za waandamanaji.

"Kwa kweli wanawake wengi nchini India wanakabiliwa na kitisho katika maisha yao katika mambo mbalimbali kama vile kunapozuka ghasia, ukosefu wa huduma za afya, kukosekana kwa usawa, kupuuzwa, lishe duni, kutojaliwa kwa afya ya mtu na utu wake"

Polisi wa kuzuia ghasia wamefunga eneo la katikati ya Delhi ili kuzuia maandamano zaidi.

Waziri mkuu wa India Manmohan Singh amesema anaelewa hasira ya wananchi, ametaka hatua zaidi zichukuliwe ili kufanya India kuwa mahali salama kwa wanawake kuishi.

Maandamano pia yamefanyika katika miji mingine ya India ikiwemo Calcutta, Bangalore na Mumbai.

Mwandishi wa BBC, India anasema kwa zaidi ya wiki mbili, mwanamke huyo ambayo hajatambulishwa amekuwa ishara ya mateso makubwa wanayopata wanawake wengi nchini humo.

Amesema, hata baada ya mazishi, mawazo yataendelea, kwa wananchi kuisukuma serikali kuchukua hatua kuhakikisha namna haki za wanawake zinavyoweza kulindwa.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.