Ghana yapiga marufuku majokofu mitumba

Imebadilishwa: 31 Disemba, 2012 - Saa 18:27 GMT

Serikali ya Ghana imepiga marufuku uagizaji wa majokofu yaliyotumika au mitumba ili kupunguza matumizi ya nishati na uchafuzi wa mazingira.

Wafanyabiashara wa majokofu Ghana

Majokofu mengi kukuu yana kemikali inayoitwa Chlorofluorocarbons (CFCs) inayoharibu mazingira.

Licha ya kuwa bidhaa hizo zimepigwa marufuku, na hazitengenezwi tena, majokofu hayo yanaaminika kutumika barani Afrika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Nishati ya Ghana ameimbia BBC kuwa marufuku hiyo, imelifanya taifa lao kuwa kielelezo katika kanda ya Afrika Magharibi.

Sheria ya kupiga marufuku majokofu hayo iliidhinishwa mwaka wa 2008, lakini muda wake uliongezwa ili kuwa na wauzaji wa bidhaa hizo kufanya marekebisho.

Hata hivyo wafanyabiashara kadha nchini Ghana wameshutumu uamuzi huo wa serikali wakisema idadi kubwa ya watu watakosa kazi.

Afisa mkuu wa tume hiyo ya nishati Alfred Ofosu-Ahenkora amesema majokofu hayo ya mitumba yanaharibu taifa hilo kwa sababu hayakutengenezwa kutumika barani Afrika na pia yanatumia kiasi kikubwa cha umeme.

Sababu ya kuyapiga marufuku

Tume hiyo imesema zaidi ya majokofu milioni mbili zilizoagizwa kutoka ng'ambo hususan kutoka mataifa ya Ulaya.

Kemikali za CFCs zimepigwa marufuku kwa mujibu wa azimio lililotiwa saini mjini Montreal Canada, kuzuia kemikali zinazoharibu tabaka la hewa ya Ozone.

Majokofu mapya kutoka Uchina

Ili kuhimiza raia wa nchi hiyo kutotumia majokofu hayo, serikali imetoa ruzuku kwa kuwapa majokofu mapya wanaorudisha ya zamani.

Mwandishi wa BBC mjini Accra anasema, sio raia wengi wa taifa hilo wanaweza kumudu gharama ya jokofu jipya, kwa hivyo mahitaji ya majokofu ya mitumba yamekuwa makubwa, katika maduka yanayouza bidhaa hiyo katika mji mkuu wa nchi hiyo.

'' Tutapoteza kazi yetu mwaka ujao, hii ndio biashara inayotupa sisi fedha za kulisha familia zetu'' alisema mmoja wa wafanyabiashara Albert Kwasi Breku.

Lakini Bwana Ofosu-Ahenkora amesema suluhisho la kudumu ni kuanzisha kiwanda cha kutengeneza majokofu nchini humo.

'' Suala la kufunga biashara za watu sio wazo zuri, ila serikali ingeliimarisha kwa kuanzisha viwanda zaidi na nadhani hilo litasaidia kubuni nafasi zaidi za kazi, badala ya kuagiza majokofu ya mitumba'' alisema Ahenkora.

Tangu kemikali ya CFCs, kupigwa marufuku, kampuni nyingi za kutengeneza majokofu zimekuwa zikitumia ina mpya inayoitwa Hydrofluorocarbons (HFCs).

Lakini mwaka uliopita ripoti ya Umoja wa Mataifa ilisema kuwa majokofu yanayotumia mfumo huo mpya wa HFCs yanatoa hewa ya sumu zaidi ambayo ni asilimia ishirini hatari zaidi kuliko hewa ya Carbon Monoxide au CO2, na hivyo matumizi ya teknolojia hiyo huenda yakaathiri mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Taifa la Ghana katika miaka ya hivi karibuni limekuwa kivutio cha mabaki ya viwanda vya kompyuta na televisheni kutoka mataifa ya Magharibi, na nyingi kati ya mabaki hayo yana sumu.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.