Waasi wa M23 watishia kususia mazungumzo

Imebadilishwa: 4 Januari, 2013 - Saa 10:09 GMT

Waasi wa M23

Mazungumzo ya kuleta amani kati ya kundi la M23 na serikali mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanarejelewa tena hii leo mjini Kampala Uganda.

Mazungumzo hayo yalisitishwa mwaka jana kwa ajili ya sherehe za Krismasi na mwaka mpya.

Hata hivyo vigogo husika kwenye mzozo huo,Rais Joseph Kabila na Jean Marie Runiga kiongozi wa kundi hilo la waasi wa M23 hawatahudhuria mazungumzo hayo.

Kundi hilo la M23 limetishia kujiondoa kwenye mazungumzo hayo hadi pale rais Joseph Kabila atakaposaini mkataba wa kusitisha mapigano.

Msemaji wa serikali ya Congo ameliambia shirika la Habari la Reuters kuwa limepuuza masharti hayo ya waasi kwa kuwa hayana msingi wowote.

Mazungumzo ya kujaribu kutatua mzozo huo uliodumu kwa zaidi ya miezi tisa yaliyofanyika mwaka uliopita yalisambaratika, baada ya wawakilishi wa pande hizo mbili kushindwa kuafikiana.

Inakisiwa kuwa zaidi ya watu laki nane wamekimbia makwao tangu waasi hao kaunzisha vita dhidi ya serikali ya nchi hiyo mwezi Mei Mwaka uliopita, kwa tuhuma za kupuuza mkataba uliokuwa sainiwa awali wa kuwashirikisha katika jeshi la serikali.

Waasi wadai kutaka kuimarisha hali ya maisha

Jean-Marie Runiga

Waasi hao ambao wanaongozwa na Bosco Ntaganda, ambaye anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita ICC, kwa madai ya uhalifu wa kivita, wamepiga hatua kubwa tangu mwaka uliopita.

Waasi hao waliuteka mji wa Goma, mwezi Novemba lakini walijiondoa kufuatia shinikizo za kimataifa.

Kiongozi wa shughuli za kisiasa wa waasi hao, Jean-Marie Runiga, aliwaambia waandishi wa habari kuwa serikali ya Congo, haikuwa imetimiza mapendekezo yake ya kusitisha mapigano na kuwa wanajeshi wa serikali wamekuwa wakijiandaa kuwashambulia.

Kundi hilo la M23 limeshutumiwa na Umoja wa mataifa kwa kufanya maasi dhidi ya raia jambo ambalo kiongozi wake Jean Marie Runiga amekanusha.

M23 imesema iataka kuimarisha hali ya maisha ya watu wa Mashariki mwa Congo, lakini Umoja wa Mataifa umedai kuwa waasi hao wanaungwa mkono na serikali za Rwanda na Uganda, madai ambayo yamekanusha vikali za serikali hizo mbili.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.