Jeshi la Ufaransa limeingia Mali

Imebadilishwa: 12 Januari, 2013 - Saa 15:17 GMT

Wanajeshi wa Ufaransa wanatumia ndege kuendelea kuwashambulia wapiganaji wa Kiislamu nchini Mali na wametuma kikosi kwenda kulinda mji mkuu wa Mali, Bamako.

Jeshi la Ufaransa nchini Mali

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian, alisema wanajeshi wamewashambulia wapiganaji waliokuwa wakielekea mji wa Mopti.

Aliongeza kusema kuwa rubani mmoja wa Ufaransa aliuwawa Ijumaa.

Naye waziri mkuu wa Ufaransa alisema Ufaransa imeingilia kati ili kuyazuwia yale aliyoyaita makundi ya ugaidi kuitisha Mali na eneo zima.

Baada ya nchi za Afrika Magharibi kuchelewa kwa miezi kadha kuingilia kati kijeshi kaskazini mwa Mali, sasa inaonesha jeshi la Ufaransa limezipiku na limeamua kuwa hakuna wakati wa kusita-sita.

Kilichoplekea ndege za Ufaransa kufanya mashambulio ni kuwa wapiganaji wa Kiislamu wamesonga kusini zaidi na kuuteka mji wa Konna, ulioko kati-kati mwa Mali, na walikuwa wanaelekea Mopti.

Hapo awali Ufaransa ilisita kutumia nguvu zake za kijeshi kwa sababu ilikuwa mkoloni wa Afrika zamani.

Ingeonekana kama inajifanya askari wa kulinda Afrika.

Algeria hasa iliionya Ufaransa isiingilie kati.

Algeria yenyenyewe imeathirika kwa sababu al Qaeda wa Afrika Magharibi wamekuwa wakifanya harakati zao katika jangwa baina ya Algeria na Mali.

Huku nyuma Jumuia ya Afrika Magharibi, ECOWAS, inaonesha nayo imeamua kufanya shime na imeidhinisha kutuma kikosi huko haraka.

Inawezekana kuwa kikosi cha Afrika Magharibi na cha Ufaransa vitajaribu kukomboa eneo la kati la Mali, kabla ya kuanza kazi kubwa ya kukomboa eneo la kaskazini.

Mazingira jangwani ni magumu wakati huu, na ndio sababu ilifikiriwa kuwa majeshi ya kigeni hayataingilia kati hadi mwezi Septemba.

Lakini pengine kwa sababu matukio yamekuwa yakibadilika haraka, ratiba hiyo ilibidi kubadilishwa.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.