Nyama ya farasi katika 'burger' Uingereza

Imebadilishwa: 16 Januari, 2013 - Saa 13:18 GMT

Maafisa wa Ireland waliofanya uchunguzi miezi miwili iliyopita, walisema bidhaa hizo ziliuzwa katika maduka kadha makubwa, yakiwemo yale ya Tesco na Iceland nchini Uingereza.

Tim Smith

Tim Smith kutoka Tesco: "Tunasikitika sana hayo yametokea"

Hata hivyo, maafisa hao walisema hamna athari zozote za kiafya kwa binadamu, na nyama hiyo iliyokuwemo katika burgers tayari imeondolewa madukani.

Maduka hayo ya Tesco yalitangaza kwamba yanajitahidi kuhakikisha "hayo hayatatokea tena".

Idara ya Uingereza inayohusika na mazingira, vyakula na masuala ya maisha ya mashambani, imetangaza kwamba inafanya kazi kwa kushirikiana na shirika linalohusika na viwango vya ubora wa vyakula (Food Standards Agency), FSA, kufanya uchunguzi wa kina kufahamu ni vipi nyama ya farasi iliweza kuchanganywa na ile ya ng'ombe.

Vile vile nyama ya nguruwe ilichanganyika na nyama ya ng'ombe.

Kwa watu ambao kidini hawaruhusiwi kula nyama ya nguruwe, kupatikana kwa chembechembe za DNA za nguruwe katika nyama ya ng'ombe itakuwa ni jambo ambalo halikubaliki kabisa.

Mkurugenzi mkuu wa FSA, amesema watafanya uchunguzi kikamilifu kutambua "chanzo cha kuchanganyika kwa nyama".

Shirika hilo la FSA pia limesema limeitisha kikao cha wawakilishi wa mashirika mbalimbali yanayohusika na vyakula kuzungumzia suala hilo.

Shirika la Ireland ambalo linahusika na vyakula, FSAI (Food Safety Authority of Ireland), pia linafanya uchunguzi kama huo, na limeeleza kwamba nyama hiyo ilitoka katika viwanda vya Jamhuri ya Ireland, vinavyofahamika kama Liffey Meats, Silvercrest na kile cha Dalepak Hambleton, katika Yorkshire ya Kaskazini.

Burgers ambazo zilikuwa na nyama ya farasi na nguruwe zilikuwa zikiuzwa katika maduka ya Tesco na Iceland nchini Uingereza na Jamhuri ya Ireland, na pia katika maduka kadha ya Dunnes, Lidle na Aldi.

Jumla ya bidhaa 27 zilizotayarishwa kwa kutumia nyama hiyo ya burgers zilikaguliwa, na 10 kati ya hizo zilikuwa na chembechembe za DNA za nyama ya farasi, na nyingine 23 zilikuwa na DNA ya nyama ya nguruwe.

Katika uchunguzi mmoja, nyama ya farasi ilikuwa ni asilimia 29 katika bidhaa za nyama ya ng'ombe Tesco.

Vile vile, bidhaa 31 za nyama ya ng'ombe zilikaguliwa katika uchunguzi huo, na 21 zilikuwa na chembechembe za DNA za nyama ya nguruwe.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.