Lance Armstrong akiri makosa

Imebadilishwa: 18 Januari, 2013 - Saa 08:51 GMT

Lance Armstrong na Oprah Winfrey

Bingwa wa mashindano ya kuendesha Baiskeli wa Marekani, Lance Armstrong, kwa mara ya kwanza amekiri hadharani kutumia dawa zilizoharamishwa aliposhinda mataji yake saba ya Tour de France.

Mwendesha baiskeli huyo mwenye umari wa miaka 41, alisema hangeweza kushinda bila madawa hayo.

Katika mahojiano yake ya kwanza tangu alipopokonywa mataji hayo, Armstrong alimuambia mtangazaji mashuhuri wa Marekani, Oprah Winfrey, kwamba yeye amekuwa na hali ya Ujanja na kigeugeu.

Lance Armstrong daima alikanusha madai kadhaa yaliyozunguka umahiri wake wa kuendesha Baiskeli kwa zaidi ya miaka kumi ya kutumia dawa za kututumua misuli.

''Ninaiona hali hii kama uongo mkubwa sana ambao niliendelea kusema mara kwa mara, nilifanya uamuzi huo , yalikuwa makosa yangu na leo niko hapa kusema pole.'' alisema Lance.

Hata hivyo alikanusha madai kuwa njama zake zilikuwa mpango mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa wa kutumia madawa yaliyoharamishwa.

Armstrong anasema hangeweza kushinda bila kutumia madawa hayo

Mahojiano hayo yalipeperushwa kwenye kituo cha televisheni cha Winfrey, mwenye umri wa miaka 58.

Katika kujibu matamshi yake, shirika la kudhibiti matumizi ya madawa yaliyoharamishwa katika michezo nchini Marekani, ilimtaka Armstrong kutoa maelezo yote kuhusiana na kashfa hii chini ya kiapo.

Mwaka jana Armstrong alipokonywa mataji yake ya mashindano ya Tour de France baada ya kusemekana kuwa mdanganyifu.

Mamilioni ya watu walimtazama Armstrong akikiri makosa yake.

Alitumia madawa ya kusisimua misuli, katika kila ushindi wake wa mashindano ya Tour De France kuanzia mwaka 1999-2005. Kwake utumiaju wa madawa hayo ilikuwa lazima kuyatumia ikiwa alitaka ushindi.

Hakuhisi kama alikuwa anadanganya wakati huo kwani aliona kama alikuwa sawa na washindani wake. Hakuhofia kukamatwa na kwamba yeye ndiye anapaswa kulaumiwa sana kwa kashfa hii.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.