Marekani yasaidia wanajeshi wa Ufaransa Mali

Imebadilishwa: 23 Januari, 2013 - Saa 08:31 GMT

Mwanajeshi wa Ufaransa akiwa kwenye harakati za kukabiliana na wapiganaji wa kiisilamu Mali

Jeshi la Marekani limeanza kuwapeleka nchini Mali kwa ndege wanajeshi wa Ufaransa pamoja na vifaa katika operesheni inayoendelea dhidi ya wanamgambo wa kiisilamu.

Ndege tano za Marekani tayari zimewasili mjini Bamako, huku ndege zengine zikitarajiwa kutua huko katika siku zijazo, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi hilo.

Ufaransa ilianza harakati zake dhidi ya wapiganaji hao wiki mbili zilizopita kwa lengo la kuwakomesha wapiganaji hao kuweza kuelekea Kusini mwa nchi.

Inajiandaa kuwakabidhi wanajeshi wa Kusini mwa Afrika hatamu za kuendelea na harakati hizo. Kikosi hicho ni cha wanajeshi 1,000 ardhini.

Takriban wanajeshi 2,000 wa Ufaransa kwa sasa wako nchini Mali huku kikosi kingine cha wanajeshi 500 wakitarajiwa kuwasili.

Kwa mujibu wa kamanda wa majeshi ya Marekani barani Afrika, ndege za kuwasafirisha wanajeshi zilianza kuondoka kutoka kambi ya jeshi Istres, Kusini mwa Ufaransa siku ya Jumanne.

Msemaji katika makao makuu ya jeshi nchini Marekani, aliambia shirika la habari la Reuters kuwa ndege tano tayari zimeondoka Ufaransa.

''Lengo letu ni kubeba, vifaa vizito kama magari ya kivita , kulingana na jeshi la Ufaransa.'' alisema msemaji wa jeshi Thierry Burkhard.

Uingereza, Belgium, Canada, Denmark na Italia pia watatoa ndege za usafiri kwa kusaidia harakati za Ufaransa dhidi ya wapigananaji.

Awali, Marekani ilisema kuwa itatoa msaada wa mawasiliano kwa wanajeshi hao.

Wenyeji wa mji wa Diabaly wakishuhudia mabaki ya vita kati ya wanajeshi wa wapiganaji

Siku ya Jumatatu, majeshi ya Ufaransa na Mali yaliteka miji miwili muhimu ya Diabaly na Douentzam, kutoka kwa wapiganaji hao baada ya wao kutoroka.

Kanali, Burkhard, alisema kuwa Ufaransa iliendelea kufanya mashambulizi ya angani katika maeneo kadhaa, ambako wapiganaji hao walikuwa wamepata udhibiti mwaka jana.

Mwezi jana, Umoja wa Mataifa, uliidhinisha mipango ya kutuma wanajeshi 3,000 wa kanda ya Afrika Magharibi kupambana na wapiganaji hao, kuweza kuteka eneo hilo zima .

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.