Pentagon yaondoa marufuku ya wanajeshi wanawake

Imebadilishwa: 24 Januari, 2013 - Saa 10:55 GMT

Makuruta wanawake wa jeshi la Marekani

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Leon Panetta, ameamua kuondoa merufuku ya wanawake wanajeshi kupigana katika mstari wa mbele.

Kwa mujibu wa afisaa mkuu wa jeshi, hatua hii inaweza ikafungua mamia ya maelfu ya nafasi za kazi kwa wanawake waweze kupigana katika mstari wa mbele, na pia kuungana na vitengo vya wapiganaji aali.

Itabatilisha amri ya 1994 iliyokuwa imewakataza wanawake kupangwa katika vikosi vya mapigano. Inategemewa kwamba uamuzi huu utatangazwa rasmi mnamo Alhamisi.

Vikosi maalum

Kuanzia mwaka huu kuna baadhi ya kazi ambazo wanawake watakubaliwa kufanya huku nyingine – zikiwemo zile za vikosi maalum na aali kama Navy Seals na Delta Force – vinaweza kuchukua muda zaidi.

Kuna uwezekano kwamba uamuzi huu utafungua zaidi ya nafasi 230,000 za kijeshi wanaopigana kwa wanawake, nyingi zao zikiwa katika vikosi vya wanajeshi wanaopigana ardhini.

Maoni

Mwenyekiti wa kamati ya huduma za kijeshi wa Senate, Carl Levin, aliunga mkono uamuzi huo. "Naliunga mkono. Linaonyesha ukweli wa hali halisi iliyopo jeshini katika Karne ya 21," alisema.

Lakini Elaine Donnelly kutoka Shirika la Marekani la Utayari wa Kijeshi aliiambia BBC kwamba uamuzi huo ulikuwa "haufai kabisa ".

"Kwa kweli jambo hilo halitawasaidia wanawake wetu walioko jeshini, wala wanaume. Kuna sababu nzuri sana kwa vikosi vinavyopigana ardhini kuwasajili wanaume tu.”

"Uingereza ililijadili jambo hili miaka kadhaa iliyopita na kuamua kwamba lilikuwa siyo jambo zuri”.

Nafasi za kazi

Vikwazo kadhaa vilitolewa mwaka mmoja uliyopita wakati Pentagon ilipofungua nafasi za kazi 14,500 zilizokuwa karibu na mstari wa mbele, kazi ambazo hapo awali wanawake walikuwa hawakubaliwi kufanya.

Wakati wa vita vya Iraq na Afghanistan, wanajeshi wa kike wa Marekani walihudumu kama maafisa wa afya, polisi wa kijeshi na majasusi.

Asilimia 14 ya wanajeshi wa Kimarekani 1.4 milioni ni wanawake.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.