Bilionea wa Afrika K kutoa mali yake

Patrice Motsepe
Image caption Patrice Motsepe

Patrice Motsepe, tajiri mkubwa zaidi wa Afrika Kusini ambaye ni Mwafrika mweusi, ametangaza kwamba atatoa nusu ya mali yake ili kuboresha maisha ya masikini.

Tajiri huyo, ambaye ni mfanyibishara wa madini, alisema kwamba Wakfu wa Motsepe ndiyo utakaoshughulikia utumiaji wa fedha hizo ili kugharamia huduma za elimu na afya.

Alisema kwamba alipewa motisha na matajiri wawili wakubwa duniani, Bill Gates na Warren Buffet, ambao huwanadi mabilionea wenzao kutoa mali yao kwa wanaohitaji.

Mzaliwa wa Soweto

"Nimekuwa nikilitafakari jambo hili kwa muda, kwamba nitatoa aghlabu nusu ya mali yangu ili kuwainua maskini na watu wengine ambao hawajiwezi Afrika Kusini. Lakini pia nilikuwa nina jukumu la kuhakikisha kwamba jambo hili lifanywe kwa njia ambayo itahifadhi maslahi ya ambao wamewekeza na mimi," Bwana Motsepe alisema katika taarifa.

Kulingana na orodha ya Forbes ya matajiri, mali ya Bwana Motsepe inagharimu dola 2.65 bilioni.

Motsepe alizaliwa mjini Soweto, ni wakili, na ni bilionea wa kwanza na pekee mweusi Afrika Kusini.

Bwana Motsepe alisema alipewa moyo na "ubuntu" – utamdaduni wa Kiafrika unaotilia mkazo utu na kusaidiana, na kwamba binadamu huwahitaji wenzao ili kunufaika kamili.