Maelfu watoroka vita kuhusu dhahabu Darfur

Image caption Vita vya 2003 vimepungua lakini makabiliano ya mara kwa mara hutokea kati ya majeshi na waasi

Mapigano makali yanaypendelea katika mgodi mmoja wa dhahabu katika jimbo la Darfur Magharibi mwa Sudan yamesababisha maelfu ya watu kuyahama makao yao .

Inaarifiwa kuwa watu wengi wanaishi nje na katika mazingira duni wakati wengine wametorokea miji ya karibu kutafuta hifadhi katika maafisi na shule ambazo zilifungwa ili kuweza kuwahifadhi.

Taarifa kutoka umoja wa mataifa zinasema kuwa wengi walioathiriwa wamelazimika kuishi nje.

Vurugu hizo ni za hivi karibuni kushuhudiwa katika eneo hilo ambalo limekuwa likikabiliwa na mizozo ya mara kwa mara

Tani mia sita za chakula zimetolewa kama chakula cha msaada pamoja na blanketi katika mji wa Al-Sireaf.

Zaidi ya watu milioni moja wamekua wakiishi katika kambi za wakimbizi wa ndani katika jimbo la Darfur baada ya mapigano ya takriban miaka kumi.

Ghasia katika jimbo la Darfur zimepungua hasa baada ya vita vilivyozuka mwaka 2003, lakini bado kuna makabiliano ya mara kwa mara kati ya majeshi ya serikali , waasi , wezi wa mifigo na makundi hasimu.

Vita vya hivi sasa vinasemekana kuwa kati ya jamii mbili za kiarabu ambazo zinazozana kuhusu migodi ya madini katika eneo la Kaskazini.

Awali Umoja wa Mataifa ulisema kuwa takriba watu 70,000 wamepoteza makao yao lakini iliweza kudurusu idadi hiyo na kuhakiki kuwa ni watu laki moja waliotoroka makwao.