Al Shabaab warejea kwa Twitter

Image caption Ukurasa wa Al Shabaab wa Twitter uliobanwa

Kundi la wanamgambo wa kiisilamu nchini Somalia, al-Shabab wameweza kufungua ukurasa mpya wa Twitter kwa lugha ya kiingereza, ikiwa chini ya wiki mbili tangu ukurasa wao wa zamani kufungwa.

Afisaa mmoja mkuu wa kundi hilo, aliambia BBC kuwa ukurasa huu mpya ni halali.

Ukurasa wa zamani wa kundi hilo ulio kwenye lugha ya kiingereza, ulifungwa baada ya kundi hilo kuutumia kutangaza mauaji ya jasusi mmoja mfaransa, na kisha kutuma ujumbe walipomuua.

Sheria za mtandao wa kijamii wa Twitter zinasema kuwa ujumbe wa vitisho kuhusu ghasia umeharamishwa , ingawa kampuni ilikataa kutoa tamko lolote kuhusu kitendo cha kufunga ukurasa huo.

Ukurasa mpya wa al-Shabab una watu 280 wanaofuatilia kundi hilo kwa karibu ikilinganishwa na ukurasa wake wa awali uliokuwa watu 20,000 waliowafuatilia.

Ulifungwa tarehe 25 mwezi Januari, wiki moja baada ya kutangaza mauaji ya jasusi wa Ufaransa Denis Allex, ambaye walikuwa wamemzuilia.

Image caption Silaha walizonaswa nazo wapiganaji wa Al Shabaab

Bwana Allex,aliyetekwa nyara nchini Somalia mwaka 2009,aliuawa na Al Shabaab kama hatua ya kulipiza kisasi baada jaribio la makomando wa Ufaransa kujaribu kumuokoa na kukosa kufanikiwa.

Wadadisi wanasema kuwa Marekani ilitaka al-Shabab kupigwa marufuku kutumia mtandao wa Twitter, ingawa haikufanikiwa kwa sababu za kisheria.

Al-Shabaab wamefurushwa kutoka miji mikubwa ya Somalia katika kipindi cha miezi 18 ingawa bado inadhibiti maeneo ya Kusini mwa Somalia.