Mustakabali wa Mali kujadiliwa Brussels

Image caption Rais wa Ufaransa Francois Hollande na makamu wa rais wa Marekani Joe Biden

Maafisa wa Umoja wa Mataifa, Muungano wa Ulaya na Afrika wanatarajiwa kukutana mjini Brussels kujadili mkakati wa kuandaa uchaguzi huru na wa kidemokrasia nchini Mali msimu wa jua.

Pia watajadili hali ya usalama na kibinadamu, hasa baada ya mapinduzi ya kiraia kufanyika mwaka jana na kufuatiwa na operesheni ya kijeshi inayoendelea dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu.

Wanajeshi wa Mali na Ufaransa, wanapambana na wapiganaji hao wanaodaiwa kuwa na uhusiano na kundi la al-Qaeda na ambao walikuwa wameliteka eneo la Kaskazini mwa Mali.

Marekani na Ufaransa, zinataka majeshi ya Afrika kutwaa udhibiti wa eneo hilo kutoka kwa wanajeshi wa Ufaransa.

Image caption Kikosi cha wanajeshi wa Mali

Wakati huohuo, ndege za kijeshi za Ufaransa, zimekuwa zikishambulia ngome za wapiganaji hao, katika sehemu za Kaskazini ili kuwazuia kupata silaha na mahitaji mengine.

Duru zinasema kuwa hatua zinazopigwa na majeshi ya ufaransa zimeweza kusababisha juhudi za kidiplomasia kuhakikisha kuwa usalama wa kudumu unapatikana Mali.

''Wakati nchi inapoporomoka, inachukua muda kuweza kuirejesha katika hali ya kawaida,'' alisema afisaa mmoja mkuu wa Muungano wa Ulaya

Akinukuliwa na shirika la habari la Reuters, afisaa huyo alisema kuwa kuna haja ya kuhakikisha kuwa eneo la Kaskazini linapata msaada wa kutosha wa kifedha ili kufadhili miradi ya maendeleo kusaidia jamii kujiimarisha.

Kikundi cha nchi za kigeni ambazo zinaunga mkono Mali, leo kitajadili namna ya kuimarisha mfumo wa kisiasa kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu ambao kaimu rais Dioncounda Traore anatumai utafanyika tarehe 31 mwezi Julai.

Pia itatizama namna ya kufadhili na kutoa mafunzo kwa kikosi cha wanajeshi 8,000 wanaotarajiwa kuchukua nafasi ya wanajeshi wa Ufaransa watakapoondoka.