Mwaka 1 jela kwa kudanganya kuhusu ubakaji

Mahakama nchini Somalia imemhukumu mwaka 1 jela mwanamke mmoja kwa kudanganya alibakwa na kundi na wanajeshi wa Somalia.

Mwanahabari aliyemhoji mwanamke huyo, pia alifungwa jela mwaka mmoja kwa kumsaidia kubuni taarifa hiyo ya kusingizia jeshi.

Wawili hao walifungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kuitusi serikali ya Somalia.

Watetezi wa haki za binadamu walilaani vikali hatua kuwakamata wawili hao na kuwafungulia mashtaka.

Siku ya Jumatatu, kampeini inayopinga dhulma dhidi ya wanawake, ilizinduliwa na mwanamke ambaye ni mashuhuri sana katika kutetea haki za wanawake , Asha Haji Elmi, ambaye pia ni mbunge na mke wa waziri mkuu, Abdi Farah Shirdon Saaid.

Majaji waliotoa uamuzi wa kesi hiyo walizingatia sana ushahidi wa kimatibabu ulioonyesha kuwa mwanamke huyo hakuwa na dalili ya kubakwa.

Kwa mujibu wa afisaa wa mahakama Ahmed Aden Farah Farah, kifungo cha jela alichopewa mwanamke huyo kitaakhirishwa kwa mwaka mmoja ili aweze kumtunza mwanawe mdogo.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesema kuwa kesi hiyo imeshinikizwa kisiasa kwa sababu mwanamke huyo alitoa madai dhidi ya maafisa wa ulinzi.

Visa vya ubakaji huripotiwa sana mjini Mogadishu,ambako maelfu ya watu walitoroka mwaka jana kwa sababu ya janga la njaa . Wengi wanaishi katika hali ya umaskini na kwenye kambi ambazo hazina ulinzi mzuri.

Majeshi ya Serikali yamekuwa yakilaumiwa kwa kufanya vitendo hivyo.