Shambulio la pili latokea Gao

Nchini Mali jeshi linasema kuwa mshambuliaji wa kujitolea mhanga amejiripua mwenyewe kwa bomu kwenye kituo cha ukaguzi katika mji wa Gao, kaskazini mwa nchi.

Shambulio hilo lilitokea Jumamosi usiku katika barabara ya kuingilia mji huo kutoka kaskazini.

Hilo ni shambulio la pili katika siku mbili zilizopita.

Ijumaa, mwanamume aliyepanda pikipiki alijiripua kwenye kituo cha ukaguzi na kumjeruhi mwanajeshi wa Mali.

Mji wa Gao ulikombolewa mwezi uliopita na wanajeshi wa Ufaransa na Mali ambao waliwatimua wapiganaji wa Kiislamu.