Martha Wangari Karua

Alizaliwa tarehe 22 Septemba mwaka 1957 mkoa wa kati. Na yeye ndiye mgombea wa pekee mwanamke katika uchaguzi huu. Aliajiriwa kama hakimu akiwa na umri wa miaka 24 kabla ya hata kuwa mbunge miaka kumi baadaye.

Mgombea wa muungano wa National Rainbow Coalition (Narc-Kenya), Karua alimteua mwanauchumi Augustine Chemonges Lotodo kama mgombea mwenza wake. Lotodo pia amewahi kuwa mbunge katika bunge la Afrika Mashariki

Karua mwenye umri wa miaka 55, alikuwa mwanachama wa upinzani ambao walipigania siasa za vyama vingi nchini Kenya mapema miaka ya tisini chini ya utawala wa rais mstaafu Daniel Moi aliyekua anaongoza kimabavu chini ya chama kimoja.

Mkereketwa wa demokrasia na maswala ya wanwake nchini Kenya, Karua alihusika na kupigania haki za wanawake kwa kutaka uungwaji mkono katika maswala yanayowahusisha wanawake wenyewe.

Karua alikuwa mfuasi mkubwa wa rais Mwai Kibaki na sera zake hadi tarehe sita Aprili mwaka 2009 wakati alipojiuzulu kama waziri wa sharia, akielezea kuwa kazi yake ilikuwa inaingiliwa sana na baadhi ya maafisa wakuu serikalini.

Aliongoza upande wa serikali wakati wa mapatano kati ya Raila Odinga na Kibaki ili kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi.

Pia aliwahi kuhudumu kama waziri wa maji aliyepigia debe sana sheria ya maji ya mwaka2002 ambayo ilichochea mageuzi katika sekta hiyo.

Karua anaahidi kuleta mageuzi katika sekta ya afya, elimu, uongozi bora kubuni nafas za kazi, kuhusisha vijana katika maswala ya uongozi na kuhakikisha serikali yake inafanya kazi kuboresha maisha ya wananchi.