Wycliffe Musalia Mudavadi

Alizaliwa tarehe 21 Septemba mwaka 1960 Magharibi mwa Kenya kutoka jamii ya waluhya.

Mwanasiasa huyu mwenye umri wa miaka 52, na ambaye siasa zake hazichangamshi sana ikilinganishwa na wanasiasa wengine, na wengi wakisema ni kwa sababu ya alivyolelewa na wazazi wake katika misingi ya kidini sana.

Mudavadi alimteua aliyekuwa mbunge Jeremiah Kioni kutoka mkoa wa kati kama mgombea mwenza wake katika chama chao cha muungano wa AMANI.

Vyama vilivyo katika muungano huo, ni kumi na tatu kikiwemo chama cha KANU chake rais mstaafu Daniel Moi. Wadadisi wanasema kuwa kuibuka kwa chama hiki huenda kukasababisha duru ya pili, ya uchaguzi na wachanganuzi wanasema Muungano wa AMANI utakuwa changamoto kwa azma ya Kenyatta na Raila.

Mudavadi alikuwa mmja wa mawaziri wakuu wawili walioteuliwa katika serikali ya Muungano kati ya Raila na Kibaki kufuatia mkataba wa amani uliofikiwa baada ya ghasia za uchaguzi.alikuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi wa mwaka 2007 kabla ya kujiuzulku ili kugombea urais mwaka huu.

Mudavadi pia alikuwa mgombea mwenza wa Uhuru katika uchaguzi wa mwaka 2002, lakini hata akashindwa katika eneobunge lake.

Hata hivyo alifufua tena azma yake ya kugombea mwaka 2005 wakati wa kura ya maoni kuhusu katiba mpya alipokuwa na upande wa (LA) ambao ulishinda dhidi ya upande wa Kibaki uliokuwa unaunga mkono rasimu ya katiba mpya.

Mudavadi anasema kuwa serikali yake, itakuwa katika mstari wa mbele kuleta mageuzi makubwa katika mfumo wa siasa pamoja na kuinua uchumi kwa manufaa ya wakenya wote.

Alisema watabdili mfumo wa kutoza kodi, pamoja na usambazaji wa rasilimali, kuhakikisha wakenya wote wataweza kupata msaada wanaostahili ili kumudu maisha yao.

Anaahidi kubuni nafasi milioni mbili za kazi, kwa kuimarisha kilimo cha minazi, ili kusaidia nchi hii kuokoa shilingi bilioni 50 za pesa za kigeni ambazo hutumia kununua mafuta ya nazi kutoka nje.