Muasi 'Kabila' afikishwa mahakani Afrika.K

Image caption Etienne Kabila alijikabidhi kwa polisi Afrika Kusini mwishoni mwa wiki

Mtu anayesema kuwa yeye ni mwanawe aliyekuwa rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Laurent Kabila, ameshtakiwa mahakamani nchini Afrika Kusini kwa njama ya kutaka kumng'oa mamlakani rais Joseph Kabila.

Etienne Taratibu Kabila, anadaiwa kuwa kiongozi wa watu wengine kumi na tisa waliofikishwa mahakamani wiki jana.

Aidha Etienne Kabila anasema kuwa rais Kabila sio mwanawe wa kweli aliyekuwa rais Laurent Kabila.

Madai yake kuhusu Rais Kabila na kuwa yeye ni mwanawe kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Laurent Kabila, yamepuuziliwa mbali na serikali ya DRC.

Etienne Kabila alijikabidhi mwenyewe kwa polisi mwishoni mwa wiki.

Hakuombwa na mahakama kukubali au kukataa mashtaka dhidi yake na kesi hiyo imeakhirishwa hadi Jumanne ambapo itajumlishwa na mashtaka dhidi ya washukiwa wengine kumi na tisa.

Viongozi wa mashtaka walisema kuwa Etienne na wenzake ni wanachama wa kundi la waasi la (Democratic Republic of Congo's Union of Nationalists for Renewal (UNR)

Wanajeshi wa kupambana na ugaidi waliwakamata washukiwa wiki jana katika mkoa wa Limpopo,chini ya sheria ya jeshi kuingilia maswala ya kigeni na ambayo wanawapa nguvu kukabiliana na shughuli za mamluki.

DR Congo, imekumbwa na uasi mkubwa wakati wote wa utawala wa Kabila.

Alichukua uongozi mwaka 2001, baada ya mauaji ya babake Laurent Kabila na ameshinda uchaguzi mara mbili