Mkuu wa tume ya uchaguzi Zimbabwe ajiuzulu

Image caption Mabango ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2008

Mkuu wa tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe amejiuzulu kwa sababu za kiafya

Hatua ya Bwana Simpson Mutambanengwe, inakuja huku Zimbabwe ikijiandaa kwa kura ya maoni kuhusu katiba mpya pamoja na uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Waziri mkuu Morgan Tsvangirai, amekuwa akishinikiza kufanyika mageuzi katika tume ya uchaguzi ili kuhakikisha kuwepo uchaguzi huru na wa haki.

Uchaguzi huo utakuwa ishara ya kumalizika kwa utawala wa serikali ya Muungano iliyoundwa baada ya ushindi wa Rais Robert Mugabe katika uchaguzi uliofanyika 2008 na uliokumbwa na ghasia na vurugu.

Bwana Tsvangirai, kiongozi wa chama cha MDC alisusia duru ya pili ya uchaguzi mwaka huo baada ya kudai kuwa alipokonywa ushindi wake katika duru ya kwanza.

Tsvangirai pamoja na Mugabe wanatarajiwa kugombea urais katika uchaguzi huo.

Chama cha Rais, Mugabe, Zanu-PF, pia kilidaawa kufanya ghasia dhidi ya wafuasi wa upinzani, madai aliyoyakanusha.

Waziri wa sheria, Chinamasa, alisema kuwa Mugabe alikubali kujiuzulu kwa Bwana Mutambanengwe, ambaye ni jaji mstaafu, aliyechukua wadhifa huo baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata mwaka 2008.

"sababu za kiafya ndizo zimempelekea kujiuzulu,'' alisema Chinamasa

Mrithi wa Mutambanengwe, atateuliwa baada ya majadiliano kati ya viongozi wa serikali ya Muungano.

Mwezi jana shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, liliitisha mageuzi katika tume ya uchaguzi , idara ya mahakama na vyombo vya habari likidai kuwa zinaunga mkono chama cha Zanu PF