Madai ya njama ya wizi wa kura Kenya

Image caption Pande zote mbili zinalaumiana kwa njama ya wizi wa kura

Serikali ya Kenya imekanusha madai kuwa kuna njama ya wizi wa kura katika uchaguzi mkuu ujao mwezi Machi 4 kwa niaba ya Muungano wa Jubilee wake Uhuru Kenyatta.

Msemaji wa serikali Muthi Kariuki alisema kuwa madai yaliyotolewa na muungano wa CORD wake waziri mkuu Raila Odinga hayana msingi na kuna hofu kuwa huenda madai hayo yakachochea hali ya wasiwasi na taharuki miongoni mwa wafuasi wa pande hizo mbili.

Alisema kuwa madai yaliyotolewa na CORD yanaleta kumbukumbu za uchaguzi wa 2007 wakati waziri mkuu na vigogo wenzake walipokuwa wanajiandaa kupinga matokeo yaliyompa ushindi Rais Mwai Kibaki.

''Ni lazima watu wafahamu kuwa mkuu wa idara ya ujasusi Julius Karangi, anayesemekana kufanya mkutano kuhusu njama ya wizi wa kura, wakati huo alikuwa nchini Uganda kwa hivyo inawezekanaje alikuwa na mkutano? alihoji msemaji wa serikali Muthui Kariuki.

Aliutaka Muungano wa Cord kutafuta sera za kuwauzia wakenya ili waweze kuwachagua badala ya kueneza propaganda na kutishia usalama wa nchi

Bwana Muriuki alisema kuwa mkuu wa utumishi wa Umma, Francis Kimemia alitoa onyo kwa wafanyakazi wa umma kuwaonya wafanyakazi wa umma dhidi ya kujihusisha na kampeini au maswala ya siasa.

Madai ya CORD yamekuja wakati pande zote mbili zinarushiana madai ya njama ya wizi wa kura. Wiki iliyopita Jubilee au upande wa Uhuru Kenyatta ulidai kuwa pande CORD wana njama ya kuwalewesha wapiga kura wao usiku mkesha wa uchaguzi.