Laurent Gbagbo afikishwa mahakamani ICC

Image caption Gbagbo ndiye rais wa kwanza wa zamani kufikishwa mbele ya mahakama ya ICC kwa kosa la uhalifu dhidi ya binadamu

Aliyekuwa rais wa Ivory Coast,Laurent Gbagbo amefikishwa katika mahakama ya kimataifa ya ICC, kujulishwa ikiwa atashtakiwa kwa kosa la uhalifu dhidi ya binadamu.

Ni rais wa kwanza wa zamani kufikishwa katika mahakama hiyo, ya Hague.

Anakabiliwa na makosa manne ikiweme mauaji na ubakaji wakati wa uchaguzi uliokumbwa na utata nchini Ivory Coast mwaka 2010.

Takriban watu 3,000 waliuawa katika ghasia hizo baada ya Gbagbo kukataa kukubali kushindwa katika uchaguzi huo.

Gbagbo mwenye umri wa miaka 67 anasisitiza kuwa hana hatia.

Mahakama inataka kuona ikiwa ushahidi uliotolewa dhidi ya Gbagbo unatosha kumfungulia kesi.

Majaji walisisitiza kuwa uamuzi wa mahakama kuhusu kesi hii hautaonyesha ikiwa Gbagbo ana hatia au la bali kuona ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kumfungulia kesi.

Mawakili wa Rais huyo wa zamani walisema tayari anachunguzwa nchini mwake na kuwa maafisa wa utawala huko ndio wanapaswa kumfungulia mashtaka wala sio mahakama ya Hague.