Jeshi la Rwanda lakanusha madai

Image caption Rais Paul Kagame

Jeshi la Rwanda limekiri kwamba linawazuia zaidi ya wanajeshi 280 katika kisiwa kimoja ziwani Kivu kwa madai ya kulitoroka jeshi.

Msemaji wa jeshi, Brigedia Jenerali Joseph Nzambwita, alisema kwamba wanajeshi hao walikuwa wanapata mafunzo upya.

Mwanajeshi mmoja, anayedai kuwa mmojawao, aliiambia BBC kwamba walihamishwa hadi kisiwani humo mwaka mmoja uliopita kutoka kwa gereza moja la kijeshi ili kuwazuia wasikutane na maafisa wa Msalaba Mwekundu waliokuwa wamepanga kuwatembelea.

Alisema wengi wao walikuwa wamezuiliwa kwa miaka mingi bila kufikisha mahakamani, na bila kukubaliwa kupokea wageni.

Akikanusha madai hayo, msemaji huyo wa kijeshi alisema BBC ilikuwa na uhuru wa kutembelea kisiwa hicho ili kuona hali halisi ilivyo.