Ndani ya uchaguzi wa Kenya

Wakenya wanakwenda kupiga kura tarehe nne mwezi Machi, uchaguzi ambao umezingirwa na kumbukumbu za uchaguzi wa mwaka 2007 uliokumbwa na ghasia . Rais Mwai Kibaki hagombei muhula mwingine , lakini mshirika wake katika serikali ya Muungano waziri mkuu Raila Odinga ni mgombea mkuu.

Ukabila

Kenya inajiandaa kwa uchaguzi mkuu ambao baadhi ya watu wanahofia kuwa huenda ukakumbwa na ghasia kama zile za mwaka 2007. Wakenya ambao idadi yao ni milioni 42, wamegawanywa kwa makundi ya zaidi ya makabila 40 na wengi hupiga kura kwa misingi ya ukabila. Baadhi ya makablila yana uhasama wa muda mrefu kuhusu swala la ardhi, maji na mifugo vyanzo vya mizozo wakati mwingi.

Uchaguzi wa 2007

Wanasiasa wengi , wanahisi kuwa njia pekee ya kufika madarakani ni kupitia miungnao ya makabila.Mwaka 2007, chama cha Raila Odinga cha ODM kiliungwa mkono na hasa watu wa kabila lake la wajaluo na majirani zao waluhya, Wakalenjin pamoja na makabila mengine. Kabila lenye watu wengi zaidi ni wakikuyu, na waliunga mkono chama cha PNU chake Rais Mwai Kibaki, wakati Kalonzo Musyoka na chama chake cha ODM-Kenya aliungwa mkono na kabila lake la wakamba.

Ghasia

Baada ya uchaguzi Odinga alisema kuwa wafuasi wa Kibaki walimuibia kura hali iliyowapelekea kufanya maandamano na ghasia. Punde baadaye,hali iliyoibuka ilikuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa misingi ya ukabila, hususan katika maeneo ya watu wengi wenye mchanganyiko wa makabila, Rift Valley, ambako wakikuyu na Kalenjin wanagombania ardhi. Wakikuyu 345 waliteketezwa hadi kufa wakiwa ndani ya kanisa mjini Eldoret. Pia kulikuwa na ghasia mbaya sana mijini Naivasha na Nakuru

Wakimbizi

Takriban watu 1,000 waliuawa na wengine laki sita kuachwa bila makao. Miaka mitano baadaye takriban watu 100,000 wangali wanaishi kambini.Kumbukumbu kama hizi zikiwa bado mbichi vichwani mwa wengi, baadhi ya watu wanahofia huenda ghasia zikazuka tena.

ICC

Wakenya wanne wanakabiliwa na kesi ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya Hague mwezi Aprili. Mmoja wa washukiwa ni Uhuru Kenyatta ambaye pia ni mgombea wa urais.Mgombea mwenza wake ni William Ruto ambaye pia anakabiliwa na kesi sawa na hiyo. Wawili hao wanashtakiwa kwa kupanga wafuasi wao kushambulia jamii hasimu mwaka 2007. Kenyatta ambaye ni mkikuyu, alimuunga mkono Rais Kibaki wakati Ruto alimuunga mkono Odinga. Wawili hao wanakanusha madai hayo vikali.