Ukatili wa polisi Afrika Kusini

Kamati maalumu ya kuangalia shughuli za polisi huko Afrika kusini inachunguza kisa ambacho dereva mmoja wa Taxi raia wa Msumbiji alifungwa nyuma ya gari la polisi na kuburutwa katika barabara za mji wa Johannesburg.

Dereva huyo aliripotiwa kufariki baadaye wakati alippokuwa kizuizini.

Picha ya Video iliyorekodiwa na mpita njia imekuwa ikionyeshwa katika vyombo vya habari vya kitaifa nchini Afrika kusini.

Shirika la Amnesty International limesema kuwa picha hiyo ni dhihirisho la hofu ambayo wamekuwa nao kwamba visa vya ukatili wa polisi vinazidi kuongezeka nchini Afrika kusini.

Msemaji wa polisi alisema alishtishwa na kisa hicho.

Vyombo vya habari vilisema kuwa polisi walimtendea ukatili dereva huyo baada ya kumtuhumu kwa kuegesha gari lake visivyo, mashariki mwa Johannesburg.