Wagombea wanakiuka sheria za kampeini Kenya

Image caption Ann Ngugi (kushoto) anasema tume ya uchaguzi ingali kuwachukulia hatua wagombea waliokiuka sheria

Shirika moja la kutetea haki za binadamau nchini Kenya (KNCHR) limekusanya maelezo kuhusu ambavyo wagombea wakuu kwenye uchaguzi wanadaiwa kutumia mbinu chafu kuwashawishi wapiga kura kuwachagua.

Inadaiwa wamewahonga wapiga kura , baadhi wametumia vibaya rasilimali za serikali pamoja na kutumia lugha ya chuki.

Shirika la kitaifa la kutetea haki za binadamu, limesema kuwa wagombea katika miungano mikuu ya cord na Jubilee, pamoja na wanasiasa kutoka vyama vingine vidogo, wamekwenda kinyume na sharia za uchaguzi wakati wakiwaomba wananchi kuwapigia kura kote nchini.

Tume hiyo inataka washukiwa kuchukuliwa hatua.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Ann Ngugi alisema kuwa ushahidi upo kwa picha za video, na picha za kawaida ambazo wamekabidhi polisi pamoja na tume ya uchaguizi , lakini idara hizo zinajikokota katika kuchukua hatua.

“Bi Ngugi alisema kuwa wameandika barua kwa tume ya uchaguzi pamoja na polisi, na walichofanya tu ni kuwaambia kwa mdomo kuwa watachukua hatua.

Kulingana na sheria inayogusia visa vya kukiuka sheria za uchaguzi, adhabu kali inaweza kutolewa kwa washukiwa ikiwa watapatikana na hatia ikiwemo kufungwa jela miaka mitatu au kutozwa faini ya shilingi milioni moja.

Ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kuwa wagombea walihusika, na visa hivyo, wanaweza kufutiliwa mbali kutoka kwa uchaguzi huo.

Bi Ngugi alisema wangali wanasubiri tume ya uchaguzi kuchukua hatua kama inavyoelezwa katika sheria za uchaguzi.