36 wauawa kwenye makabiliano DRC

Image caption Maelfu ya watu wameachwa bila makao kufuatia mapigano kati ya jeshi na waasi wa M23

Takriban watu 36 wameuawa katika makabiliano makali kati ya waasi na jeshi Mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Taarifa hizi zimethibitishwa na jeshi la Congo pamoja na Umoja wa Mataifa.

Zaidi ya watu 3,000, wametafuta makao mapya karibu na kambi ya Umoja wa mataifa katika eneo la Kitchanga katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Waasi wa kundi la APCLS, walivamia mji wa huo wakiwalenga watu wa jamii ya kinyarwanda wanaoonekana kuwaunga mkono wapiganaji wa M23

Takriban watu 800,000, wametoroka mapigano, ambayo yamekuwa yakiendelea tangu kuanza kwa harakati za kundi la M23 mwezi Mei mwaka jana.

Kundi hilo, liliteka mji wa Goma kwa muda mwezi Novemba, lakini umekumbwa na mapigano wiki hii.

Mnamo Jumapili, viongozi wa Afrika walitia saini makubaliano ya amani yaliyoshinikizwa na Umoja wa mataifa ili kumaliza vita nchini humo.

Mlinda amani mmoja wa Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa watu 50 waliojeruhiwa kwenye makabiliano hayo.

Duru za kijeshi zilisema kuwa nyumba 30 ziliteketezwa wakati wa makabiliano hayo.

Wakati huohuo, kundi la M23 linasema kuwa limemfuta kazi kiongozi wake wa kisiasa Jean-Marie Runiga, wakimtuhumu kwa kosa la uhaini.

Mapema wiki hii, takriban watu 8 waliuawa kwenye makabiliano mjini Rutshuru takriban umbali wa kilomita 70 kutoka mji wa Goma.