Ghasia zazuka mjini Conakry, Guinea

Wafanyakazi wa mashirika ya misaada nchini Guinea wanasema mtu mmoja ameuwawa na wengine kadha kujeruhiwa pale askari wa usalama walipofyatua risasi mbele ya watu katika mtaa wa Koloma wa mji mkuu, Conakry.

Hayo yanafuatia ghasia mjini humo kati ya wafuasi wa upinzani, askari wa usalama na makundi ya kikabila.

Upinzani umekuwa ukiandamana dhidi ya uchaguzi unaopangwa kufanywa mwezi May.

Upinzani unasema serikali itafanya udanganyifu kwenye uchaguzi huo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito wa amani nchini Guinea, ambako kumekuwa na ghasia za kisiasa na kikabila kwa miaka kadha.