Malkia Elizabeth alazwa hospitalini

Image caption Malkia Elizabeth

Malkia Elizabeth wa Uingereza amelazwa hospitali mjini London akiwa anaugua tumbo. Alipelekwa hospitalini mwishoni mwa juma lililopita.

Taarifa kutoka makao yake ya Kasri la Buckingham zinasema kuwa shughuli zote rasmi za malkia zimeahirishwa ama kufutwa, ikiwa ni pamoja na ziara aliyotarajia kufanya mjini Roma.

Malkia Elizabeth, mwenye umri wa miaka 86, alipelekwa hospitali ya King Edward VII baada ya kuonyesha dalili za ‘gastroenteritis’, Kasri la Buckingham lilisema. ‘Gastroenteritis’ husababisha uvimbe tumboni.

Kasri la Buckingham lilisema kwamba hali ya malkia ilikuwa siyo mbaya, na kwamba alikuwa hajalala kitandani, bali alikuwa anatembeatembea.

Hii ni mara yake ya kwanza kulazwa kwa muda wa miaka 10 iliyopita, na inategemewa kwamba atabaki hospitali kwa uchunguzi kwa siku mbili zijazo.