Marekani yaihidi Misri mamilioni ya fedha

Image caption Bwana Kerry na Rais Morsi waongea

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, ameahidi kuipa Misri dola 450 milioni ili kuinua uchumi wa nchi hiyo unaozidi kuzorota. Hata hivyo alisema kwamba "kazi zaidi inahitajika kufanywa".

Bwana Kerry, aliyefanya maongezi na Bwana Morsi nchini Misri, alimwambia ahakikishe kwamba uchaguzi wa mwezi Aprili utafanyika chini ya mazingira ya haki na uwazi.

Uchaguzi huo umeshasusiwa na chama kikuu cha upinzani, huku maandamano yakizidi kukithiri.

Chama cha National Salvation Front kinasema kwamba sheria za uchaguzi zinampendelea Rais Morsi – dai ambalo yeye analikanusha.

Mkopo

Misri imegawanyika kati ya Waisilamu wenye siasa kali na wapinzani wenzao wenye siasa za wastani.

"Ni wazi kwamba juhudi zaidi zinahitajika kufanywa nchini Misri ili umoja, amani na ukuzaji uchumi udumishwe," Bwana Kerry alisema baada ya mazumgumzo hayo ya Jumapili.

"Nimesema hivi katika mikutano yangu yote: ya kwamba Wamisri waliokuwa hawana woga na waliokesha huko Tahrir (Cairo) hawakuweka maisha yao hatarini ili tu kuona juhudi zao za kuhakikisha maisha mazuri ya baadaye nchini Mirsi zikipuuzwa."

Awali, Bwana Kerry alitoa wito kwa serikali ya Misri kukubalinana na shirika la fedha la IMF ili kupata mkopo wa dola 4.8 bilioni ambao utaweza kuisababisha Marekani kuipa Misri fedha zaidi.