Polisi Afrika Kusini kufikishwa kortini

Image caption Mido Macia akiburuzwa nyuma ya gari la polisi

Polisi wanane wa Afrika Kusini wanategemewa kufikishwa mbele ya mahakama kuhusiana na kisa cha wiki iliyopita ambapo mtu mmoja, raia wa Msumbiji, aliburuzwa nyuma ya gari la polisi.

Mido Macia, 27, alifariki kutokana na majeruhi aliyopata kichwani na alipovuja damu mwilini, baada ya kukamatwa huko Daveyton, mashariki mwa Johannesburg.

Uchunguzi ulifanywa baada ya video kufichuliwa iliyoonyesha mwanamume mmoja aliyefungwa pingu akiburuzwa.

Rais Jacob Zuma alisema tukio hilo lilikuwa "baya sana" na "lisilokubalika".

Maafisa hao Ijumaa iliyopita walifunguliwa mashataka ya mauaji, siku tatu baada ya tukio hilo.

Bwana Macia, dereva wa magari madogo ya abiria, alikamtawa kwa madai ya kuegesha gari lake mahala ambapo alizuia magari mengine.

Kanda hiyo ya video inasemekana ilikchukuliwa na mpita njia kwa simu ya rununu. Watu walighadhabishwa sana baada ya picha hiyo kuonyeshwa katika televisheni.