Soka na wapenzi wa jinsia moja Nigeria

Image caption Rashidi Williams ambaye ni mwanaharakati anasema ni vigumu kuishi kama mwanaume anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja Nigeria

Shirikisho la soka duniani, Fifa limeliandika barua shirikisho la soka Nigeria kuhusu madai kuwa wanawake wapenzi wa jinsia moja wamepigwa marufuku kucheza soka nchini humo.

Dilichukwu Onyedinma, mwenyekiti wa soka ya wanawake nchini Nigeria, alinukuliwa akitoa matamshi hayo.

"mchezaji yeyote anayejihusisha na mapenzi ya jinsia moja atatupiliwa mbali,'' alinukuliwa akisema Dilichukwu.

Matamashi yake yanakiuka sera ya ubaguzi ya shirikisho la soka duniani FIFA lakini pia ushoga ni jambo linalokatazwa na sheria za nchi hiyo.

Mwanaharakati, Rashidi Williams anasema kuwa ni vugumu sana kuishi Nigeria kama mwanaume anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Kwa sasa mswaada unaoharamisha ndoa za jinsia moja, unasubiri kutiwa saini na rais wa nchi hiyo Goodluck Jonathan ili kuwa sheria.

Ikiwa jambo hili litafanyika, mkusanyiko wa wapenzi wa jinsia moja au msaada wowote kwa mashirika yanayotetea haki zao iwe kwa siri au wazi, itapigwa marufuku, huku watakaopatikana na hatia wakifungwa jela miaka 14.

Katika hotuba yake hivi karibuni Bi Onyedinma aliripotiwa akisema kuwa wanawake wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja hawataruhusiwa kucheza katika timu ya taifa na kwamba wataondoshwa katika soka ya vilabu.