Viongozi wa dunia wampongeza Papa mpya

Image caption Pongezi nyingi kumiminiwa Papa mpya

Habari zaidi, viongozi wa kutoka mataifa ya Latin Amerika, wamekuwa wakituma pongezi zao kwa Papa mpya mteule wa kanisa Katoliki Francis 1. Papa huyo anatokea nchi ya Argentina, na anakuwa Papa wa kwanza kutoka sehemu hiyo.

Argentina, ikiwa ndio asili ya Papa, ilikuwa na sababu kubwa zaidi kusherehekea uteuzi wake. Licha ya uhusiano wa msuguano kati ya rais wa Argentina, Christina Fernandez, alikuwa wa kwanza kutuma pongezi kwa Papa Francis, huku akimtakia kila kheri katika kupigania haki na usawa.

Wawili hao waliwahi kutofautiana hadharani juu ya suala la ndoa ya watu wa jinsia moja.

Image caption Rais wa Argentina

Nchini Brasil, inayotazamiwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya waumini wa kanisa hilo la Roma duniani, rais Dilma Rousef alimpongeza sana Papa Francis, na kwa jumla wananchi wa Argentina. Pia alimkaribisha Papa Francis kwa moyo mkunjufu kuhudhuria sherehe za kuadhimisha siku ya vijana duniani mnamo Julai, mjini Rio.

Kwa rais wa Chile, Sebastian Pinera alisema kuwa ameridhishwa na kuwa Papa huyo mpya anaielewa nchi ya Chile vizuri sana na hata akamkaribisha kuja kuzuru tena.

Rais wa Colombia Juan Manuel Santos, yeye alifurahishwa zaidi na kuwa kwa Mara ya Kwanza wamepata Papa ambaye lugha yake ya mama ni Kispania.