Rais Barack Obama kufanya ziara Israel

Image caption viongozi wa Marekani na Israel washauriana

Rais Barack Obama anatarajiwa kuwasili nchini Israel Jumatano , ikiwa ni ziara yake ya kwanza nchini humo tangu kuwa rais wa Marekani. Miongoni mwa masuala makuu yanayaotarajiwa kujadiliwa ni pamoja na Iran, mapigano nchini Syria, na mzozo kati ya Israel na Palestina.

Ziara ya Obama inajiri huku akishutumiwa na baadhi kwa kuwa hajazuru Israel katika muhula wake wa kwanza kama rais. Wakosoaji wake wamehoji kuwa hiyo ni ishara tosha kuonyesha ushirikiano wake na taifa hilo sio wa karibu.

Utawala wake umeelezea kuwa kuna ushirikiano thabiti na Israil.

Israel na Palestina je?

Image caption bendera za Israel na Palestina

Lakini kuhusu uhusiano kati ya Israel na Palestina, Obama amesema anaenda bila mpango wowote maalum, na kwa kusema hivyo ni njia moja ya kupunguza matumaini ya watu.

Baadhi ya watu wanahoji kuna uwezekano wa mashauriano kuanzishwa upya ingawaje ni wachache sana wanaoamini kwamba wakati wa kufanya hivyo ni sasa.

Image caption Obama na Netanyahu

Uhusiano wa rais Obama na waziri mkuu wa Israil Benjamin Netanyahu umekuwa na changamoto zake na kura ya maoni iliofanywa hivi maajuzi ilionyesha ni asilimia kumi tu ya raia wa Israel ambao wana imani na rais Obama.

Wengi watakuwa wanasubiri kwa hamu hotuba akayotoa rais Obama kwa raia wa Israel.