Polisi SA adaiwa kumuua mchimba migodi

Polisi wa Afrika Kusini

Polisi mmoja Afrika Kusini amedai kwamba mwenzake alimuua mchimba migodi aliyekuwa kajeruhiwa wakati wa migomo katika mgodi wa Marikana mwaka uliopita.

Hendrick Myburgh aliliambia jopo la uchunguzi kwamba alisikia mlio wa risasi halafu akamwona mwenzake kasimama karibu na mwili wa mchimba migodi aliyekuwa hai dakika chache kabla.

Wachimba migodi 34 wa Marikana walifariki baada ya polisi kuwafyatulia risasi. Polisi wanasema kwamba walikuwa wanajikinga kwa kufanya hivyo.

Baada ya kisa hicho wachimba migodi 270 walitiwa mbaroni na kufunuguliwa mashtaka ya mauaji, lakini baadaye mashtaka hayo yalitupiliwa mbali.

Awali, mashahidi waliwalaani maafisa wa polisi kwa kuwapiga risasi wachimba migodi waliojeruhiwa au waliokuwa wameshafungwa pingu. Hata hivyo hii ni mara ya kwanza kwa polisi nao kusema hivyo, waandishi wanasema.

Kisa hicho kilitokea mnamo 16 Agosti 2012, baada ya juma zima la migomo. Mahakama inachunguza vifo vyote 44.