Kikosi maalum cha Umoja wa mataifa DRC

Image caption Wanajeshi wa UN walioko Goma wanashutumiwa kwa kushindwa kuangamiza makundi ya waasi

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limeidhinisha kuundwa kwa kikosi maalum cha jeshi kitakachokuwa kikiendesha operesheni dhidi ya makundi yaliyojihami mashariki mwa DRC.

Ni mara ya kwanza kwa Umoja wa mataifa kutoa mamlaka kwa kikosi chake kufanya mashambulizi na kuwapokonya waasi silaha.

Kikosi hicho kitakuwa na wanajeshi 2,500 watakaOpambana na waasi na kuwapokonya silaha.

Kile kikosi kilichopo sasa cha wanajeshi 20,000, kinalinda amani na kimekuwa kikishutumiwa kwa kutofanya kazi vyema kiasi cha kushindwa kumaliza vita vilivyodumu zaidi ya miaka kumi.

Wanajeshi kutoka Tanzania, Msumbiji na Afrika Kusini, watajumuisha sehemu kubwa ya kikosi hicho, kitakachoanza kazi mwezi Julai.

Madini mengi ya nchi hiyo yameporwa na makundi mengi pamoja na nchi zingine wakati wa mzozo huo.

Azimio hilo limeungwa mkono na wanachama wote wa baraza la usalama , limesema kuwa kikosi hicho kipya kitafanya kazi kwa nguvu ili kuzuia kusambaa kwa makundi ya waasi na kuyapokonya silaha.

Kikosi cha kulinda amani kimekuwa DR Congo kwa zaidi ya miaka kumi na wakati huo kilikuwa kikosi kikubwa zaidi cha wanajeshi duniani

Mwezi jana viongozi wa kikanda walitia saini mkataba wa amani ulioafikiwa na Umoja wa mataifa kumaliza vita vya DRC

Takriban watu 500,000 wametoroka makwao tangu kuanza kwa uasi wa kundi la M23 mwezi Aprili mwaka jana.