Cameron ampongeza Kenyatta

  • 30 Machi 2013

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron imetoa taarifa iliyosomwa na msemaji baada ya hukumu ya mahakama makuu ya Kenya kuamua kuwa Uhuru Kenyatta ameshinda kihalali uchaguzi uliofanywa awali mwezi March.

Msemaji alieleza kuwa waziri mkuu amemuandikia rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Jumamosi.

Alimpa hongera yeye pamoja na wengine waliochaguliwa ambao ushindi wao ulikubaliwa na mahakama makuu Jumamosi.

Alisistiza kuwa hii inamaanisha mwisho wa mchakato uliokuwa muhimu, ambapo wananchi wengi kabisa walijitokeza kupiga kura kushinda wakati wowote ule.

Waziri Mkuu aliwasihi Wakenya wajivunie ishara waliyopeleka kwa ulimwengu kuonesha azma yao ya kutumia fursa yao katika demokrasi.

Alisema watu wa Kenya wameamua kuonesha uhuru wao na kutatua mizozo kisheria na kwenye taasisi imara ya mahakama makuu, na katiba.

Waziri Mkuu Cameron piya alisistiza kuwa Uingereza imeazimia kuendeleza ushirikiano baina yake na Kenya.

Ameelezea uhusiano baina ya Uingereza na Kenya ni wa kihistoria na wa kina, na anatazamia kufanya kazi pamoja na serikali mpya ya rais mteule.